Nenda kwa yaliyomo

Mto Medjerda

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mto Medjerda unavyoonekana nchini Tunisia

Mto Medjerda (kwa Kiarabu: وادي مجردة, unajulikana pia kama Wadi Majardah au Mejerda; hapo zamani kama Bagradas) ni mto uliopo upande wa kaskazini mwa Afrika unaotiririka kutoka kaskazini-mashariki mwa Aljeria kupitia Tunisia kabla ya kuishia katika Ziwa la Tunis. Mto huu una urefu wa takribani kilomita 460 (sawa na maili 290), na ndio mto mrefu zaidi nchini Tunisia.[1]

Ukubwa wa mto

[hariri | hariri chanzo]

Mto Medjerda unaanzia katika Milima ya Tell Atlas, ambayo ni sehemu ya Milima ya Atlas kaskazini-mashariki mwa Aljeria, na kisha unatiririka kuelekea upande wa mashariki kuingia nchini Tunisia kabla ya kumwaga maji yake katika Bahari ya Mediterania kupitia Shoroba ya Utica. Mto huu una umuhimu mkubwa sana wa kiuchumi nchini Tunisia ambapo umejengwa mabwawa katika maeneo kadhaa, ukiwa chanzo kikuu cha maji yanayotumika kumwagilia mashamba ya ngano nchini humo.[2]

Kijiografia, Shoroba ya Utica ilitengenezwa miaka 6,000 iliyopita baada ya kipindi cha barafu kuisha. Baada ya muda, mchanga na matope yaliyosombwa na Mto Medjerda yalijaza sehemu ya kaskazini ya shoroba hiyo. Tafiti za kijiografia na picha za setilaiti zinaonyesha kuwa mabadiliko haya ya mandhari ya ardhi yamekuwa yakitokea kwa miaka 3,000 iliyopita, ambapo bahari ilirudi nyuma na kuacha rasi ya Ghar el Melh kama kumbukumbu pekee ya shoroba ya zamani ya Utica. Kufuatia mafuriko makubwa ya mwisho yaliyotokea mwaka 1973, Mto Medjerda ulibadilisha mwelekeo wake na sasa unatiririka kupitia mtaro maalum uliochimbwa hapo awali kwa ajili ya kupunguza kasi ya maji ya mafuriko.[3]

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Kihistoria, Mto Medjerda umekuwa njia muhimu sana ya maji nchini Tunisia, ukisambaza maji safi kwa miji mikubwa na jamii zinazoishi kando yake. Maji yake yanayotumika kwa umwagiliaji ni uti wa mgongo wa kilimo katika ukanda huo mzima.

Kutokana na kuwa rasilimali ya kimkakati, mto huu uligombaniwa na kutawaliwa mara nyingi na falme mbalimbali za kihistoria wakiwemo Wacarthage, Waroma, Wavandali, Wabyzantine, Waarabu, na Waturuki wa Osmani. Miji kadhaa mikubwa ilianzishwa kando yake ikiwemo Utica, Carthage, na mwishowe Tunis. Hata hivyo, bandari za zamani za Utica na Ghar el-Melh zilifungwa kabisa baada ya bandari hizo kujaa mchanga na tope zilizosombwa na mto huu kwa miaka mingi.

  1. ↑ Beschaouch, Azedine (1986). "De l'Africa latino-chrétienne à l'Ifriqiya arabo-musulmane: questions de toponymie". CRAI (kwa Kifaransa). 130 (3): 530–549. doi:10.3406/crai.1986.14420. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2024-01-28. Iliwekwa mnamo 2023-10-08.
  2. ↑ "Study on Integrated Basin Management of the Medjerda River | Tunisia | Countries & Regions | JICA". www.jica.go.jp (kwa Kiingereza). Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 19 Oktoba 2009. Iliwekwa mnamo 28 Julai 2017.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. ↑ Ameur Oueslati, Faouzia Charfi & Fadhel Baccar, La basse vallée de Oued Majerda et la lagune de Ghar El Melh, projet WADI
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mto Medjerda kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.